Thursday, January 16, 2014

Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki na Sheria za Kanisa ni matunda endelevu ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican



Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, Tanzania katika mahojiano maalum na Radio Vatican kuhusiana na Maadhimisho ya Mwaka wa Imani anabainisha kwamba, Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki: muhtasari wa: Imani, Sakramenti za Kanisa, Maisha Adili na Maisha ya Sala pamoja na Sheria Mpya za Kanisa ni matunda ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, ambayo Mama Kanisa anaona fahari kuyaadhimisha katika Mwaka huu wa Imani uliotangazwa na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI. RealAudioMP3
Hati kumi na sita za Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican ni dira na mwongozo katika maisha na utume wa Kanisa Katoliki katika ulimwengu mamboleo. Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican ulikuwa ni Pentekoste mpya kwa Kanisa, licha ya mapungufu yanayoendelea kuoneshwa na Watoto wake, lakini bado Kanisa limesimama kidete kuwa kweli ni Mwanga wa Mataifa, Mhimili wa Ukweli na Mtetezi makini wa wanyonge na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Kanisa limekuwa ni Mama na Mwalimu anayetumia rehema, upendo na majadiliano katika mikakati yake ya kichungaji kwa Familia ya Mungu.
Kardinali Polycarp Pengo anasema kwamba, Baba Mtakatifu Yohane wa Ishirini na tatu katika hotuba yake alikazia kwa namna ya pekee “aggiornamento” Upyaisho wa maisha na utume wa Kanisa. Lengo likiwa ni kulinda na kufundisha hazina takatifu ya Mafundisho ya Kanisa kwa namna iliyo bora zaidi na kwa ajili ya watu wote kwa kugusa Nyanja zote za maisha ya mwanadamu. Mababa wa Mtaguso walipania kwa namna ya pekee kujenga na kudumisha umoja, upendo na mshikamano kati ya watu.
Mwaka wa Imani ufumbue macho ya Familia ya Mungu ili kuona: mafanikio, matatizo, changamoto na fursa zilizopo kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa bila hata ya kukata tama bali kuendelea kuwa na imani na matumaini kwa Kristo, kichwa cha Fumbo la Mwili wake, yaani Kanisa linaloongozwa na Roho Mtakatifu.
Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki ni zawadi na chombo makini cha Uinjilishaji Mpya. Waamini wajitahidi kusoma alama za nyakati kwa kujikita zaidi na zaidi katika maisha ya: Imani, Sakramenti za Kanisa, Maadili na Sala. Imani anasema Kardinali Polycarp Pengo Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam kwamba, inamwilishwa katika matendo.
Imetarishwa na Padre Richard Mjigwa, C.PP. S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 


Habari : Radio vatican

No comments:

Post a Comment