Thursday, January 16, 2014

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Siku ya 22 ya Wagonjwa Duniani kwa Mwaka 2014



Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 11 Februari anaadhimisha Siku ya Wagonjwa Duniani sanjari na Siku kuu ya Bikira Maria wa Lourdes. Mwaka 2014 Siku ya Wagonjwa Duniani itaongozwa na kauli mbiu " Imani na Upendo: imetupasa na sisi kuutoa uhai wetu kwa ajili ya hao ndugu" I Yoh. 3:16.

Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu Francisko anapenda kutoa ujumbe huu kwa wagonjwa na wahudumu wa wagonjwa kutoka sehemu mbali mbali za dunia, kutambua kwamba, wao ni kielelezo makini cha Kristo anayeteseka na kwamba, wanabeba pamoja na Kristo mahangaiko yao ya ndani.

Kwa njia ya Fumbo la Msalaba, Mwana wa Mungu amebomoa upweke wa mahangaiko na kutoa mwanga angavu, kielelezo cha Fumbo la Upendo wa Mungu linaoimarishwa kwa njia ya mwanga wa Pasaka, tayari kuwa na ujasiri wa kupambana na mahangaiko ya ndani kwa kutambua kwamba, Yesu yuko pamoja nao katika mapambano haya!

Baba Mtakatifu anasema kwamba, kwa njia ya Fumbo la Umwilisho, Mwenyezi Mungu hakuondoa hali ya magonjwa na mahangaiko katika maisha ya mwanadamu, bali amejitwalia katika mwili wake, akayageuza na kuyapatia maana mpya na maisha mapya, ili kwa kuungana na Kristo mateso na mahangaiko haya yaweze kupata mwelekeo chanya.

Yesu ni njia na kwa nguvu za Roho Mtakatifu, waamini wanaweza kupata ujasiri wa kumfuasa. Mwenyezi Mungu amemkirimia Mwanaye wa pekee pendo ambalo amewamegea pia wanadamu, ili waweze kupendana wao kwa wao na kuthubutu kutolea maisha yao kwa ajili ya jirani zao.

Baba Mtakatifu anasema, imani kwa Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo inakuwa ni nguvu; imani kwa Yesu Kristo aliyeteswa inakuwa pia ni nguvu ya kupenda hata adui. Mtihani wa imani kwa Kristo ni zawadi ya mtu kutolea maisha yake kwa ajili ya jirani zake, hasa wale ambao ni maskini na wanyonge!

Kwa njia ya sakramenti ya Ubatizo na Kipaimara, waamini wanaalikwa kujifananisha na Kristo, Msamaria mwema kwa wote wanaoteseka na kusumbuka kwani katika hili, waamini wamelifahamu pendo la Kristo, kwa kuwa Yeye aliutoa uhai wake kwa ajili yao, nao imewapasa kuutoa uhai wao kwa jili ya hao ndugu.

Lengo ni kuwaonjesha wagonjwa matumaini na tabasamu la Mungu kati ya Watu wake. Ukarimu unapaswa kuwa ni sehemu ya majitoleo ya waamini kwa ajili ya watu wanaoteseka, kwa kuwaonjesha joto la upendo unaobubujika kutoka katika Moyo Mtakatifu wa Yesu, ili kushiriki kikamilifu katimka ujenzi wa Ufalme wa Mungu.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa siku ya ishirini na mbili ya wagonjwa duniani kwa Mwaka 2014, anawalika waamini kukua na kukomaa katika upendo unaoheshimu na kujali, kwa kuangalia na kuwakirimia wengine usalama wa maisha. Bikira Maria alikuwa msikivu makini wa Neno la Mungu na mahitaji ya watoto wake.

Bikira Maria kwa kusukumwa na huruma ya Kimungu ndani mwake, anajisahau na kutoka mbio kuelekea Galilaya ili kukutana na binamu yake Elizabeth; alikuwa makini kusikiliza kilio cha Wanaharusi wa Kana, walipotindikiwa na divai wakati wa sherehe; anabeba ndani mwake katika hija ya maisha yake, maneno ya utabiri wa Mzee Simeoni kwamba, upanga utautoboa moyo wake; kwa nguvu ya ajabu anadiriki kusimama chini ya Msalaba wa Yesu.

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kumkimbilia Bikira Maria kwa imani, matumaini na ibada kwa kutambua kwamba, atawasikiliza na kuwasaidia na kamwe hatawaacha! Bikira Maria ni Mama wa Yesu Msulubiwa, aliyefufuka kutoka katika wafu: anayeendelea kuwa pembeni mwa misalaba ya maisha ya wafuasi wake na kuwasindikiza katika hija ya ufufuko na utimilifu wa maisha.

Baba Mtakatifu anasema kwamba, Mtakatifu Yohane alikuwa na Bikira Maria chini ya Msalaba, anawasaidia waamini kutambua chemchemi ya imani na mapendo yanayobubujika kutoka katika moyo wa Mungu ambaye ni Upendo. Anawakumbusha waamini kwamba, hawawezi kumpenda Mungu bila kuwapenda jirani zao. Yeyote anayesimama chini ya Msalaba pamoja na Bikira Maria anajifunza kupenda kama Yesu. Msalaba ni uhakika wa upendo aminifu wa Mungu kwa ajili ya binadamu.

Ni upendo unaoingia katika dhambi na kusamehe; unagusa mateso na mahangaiko ya binadamu na kuwakirimia nguvu za kuweza kustahimili; anaingia katika kifo, ili kukishinda na kuokoa... Msalaba wa Kristo unawaalika waamini kujiachilia ili waweze kuguswa na upendo wa Mungu; kuangalia kwa huruma na mapendo, hasa wale wanaoteseka na wanaohitaji msaada.

Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha ujumbe wake kwa Siku ya 22 ya Wagonjwa Duniani kwa Mwaka 2014 chini ya maombezi ya Bikira Maria, ili awasaidie wagonjwa waweze kuishi mateso na mahangaiko yao kwa kuungana na Yesu Kristo; awasaidie wale wanaowatunza wagonjwa kutekeleza wajibu wao barabara. Baba Mtakatifu anatoa baraka zake za kitume kwa wagonjwa na wafanyakazi wote katika sekta ya afya.

Ujumbe huu umetafsiriwa na
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

No comments:

Post a Comment