Thursday, January 16, 2014

Ujumbe wa Papa Francisko kwa ajili ya kuombea amani kwa Mwaka 2014



Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake wa Siku ya 47 ya Kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2014 sanjari na Maadhimisho ya Siku kuu ya Bikira Maria Mama wa Mungu, anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kujikita katika udugu ambao ni msingi na njia ya amani, ili kuondokana na dhana ya chuki, kinzani na uadui mambo yanayomsababishia mwanadamu majanga mbali mbali ya maisha. RealAudioMP3

Watu waheshimiane na kuthaminiana kama ndugu, kwani udugu ni tunu msingi ya ubinadamu katika kukuza na kudumisha mahusiano. Bila ya kujenga na kudumisha udugu ni vigumu sana kujenga jamii inayosimikwa katika haki na amani na badala yake, watu watajikuta wanamezwa na utandawazi usiojali wala kuguswa na shida za jirani. Watu wana kiu ya kutaka kuona zawadi ya uhai, haki msingi za binadamu na uhuru wa kidini vikiheshimiwa; wanataka kusikia kwamba, biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo vimekomeshwa na kwamba, hakuna tena vita duniani na kinzani duniani, mambo yanayoleta athari kubwa kwa maisha na maendeleo ya watu.

Utandawazi umewafanya watu wajisikie kuwa dunia imekuwa kama kijiji, lakini hauwasaidii kujenga na kuimarisha dhana ya udugu, ndiyo maana kuna tofauti na kinzani; kuna umaskini na ukosefu wa haki msingi za binadamu pamoja na ukosefu wa utamaduni wa mshikamano wa dhati. Watu wamemezwa mno na ubinafsi pamoja na malimwengu, kiasi cha kuwabeza maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Mifumo ya maadili kijamii bado haijafanikiwa kujenga udugu na mshikamano wa dhati kwa kutambua kwamba, wote ni watoto wa Mwenyezi Mungu wanaopaswa kuwa majirani na ndugu wanaohudumiana.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake unaofumbata utajiri mkubwa wa Maandiko Matakatifu, anazungumzia kuhusu kazi ya uumbaji na uwepo wa Familia ya kwanza ya binadamu na jinsi ambavyo wivu wa Kaini ulivyopelekea mauaji ya Abeli ndugu yake. Hapa ukawa ni mwanzo wa kuvunjika kwa msingi wa udugu kadiri ya mpango wa Mungu na hatimaye, kuibuka usaliti na ubinafsi; chanzo cha ukosefu wa haki msinghi ndani ya Jamii.

Baba Mtakatifu anawakumbusha waamini kwamba, kwa njia ya Yesu Kristo, wote wamekuwa ni ndugu hali inayojenga mchakato wa kudumisha umoja na udugu kati ya watu. Kwa njia ya Fumbo la Msalaba, kielelezo cha hali ya juu kabisa cha upendo wa Mungu kwa binadamu, Yesu alivunjilia mbali utengano kati ya watu, akaanzisha Agano Jipya, linalowapatanisha binadamu wote na hivyo kujisikia kuwa ni watoto wa Baba mmoja na amani ya binadamu katika umoja wao! Fumbo la Msalaba linawawajibisha binadamu kutaabikiana na kusumbukiana katika maisha.

Baba Mtakatifu anasema udugu ni msingi na njia ya amani ni sehemu ya Mafundisho Jamii ya Kanisa kwani amani ni jina jipya la maendeleo endelevu yanayogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Mataifa hayana budi kujenga na kuimarisha moyo na ari ya udugu, kwa ajili ya mafao ya wengi na kama sehemu ya muendelezo wa haki jamii; mshikamano unaoratibiwa na kanuni auni.

Uchu wa mali na madaraka ni chanzo cha kinzani, migogoro na vita sehemu mbali mbali ya dunia. Viongozi badala ya kujikita katika dhana ya huduma, wanageuka na kuwa ni wanyonyaji na wanyanyasaji, changamoto ya kuwa na mwelekeo mpya wa kupenda na kuhudumia kwani wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Baba Mtakatifu anasema, udugu ni jambo muhimu sana katika mapambano dhidi ya umaskini duniani kwa kujenga na kuimarisha mshikamano wakati wa furaha na raha; wakati wa shida na magumu, kwani haya yote ni sehemu ya maisha ya mwanadamu. Umaskini wa hali na kipato unaendelea kuongezeka siku hadi siku, changamoto ya kuchuchumilia mshikamano wa kidugu, kwa kukazia: haki msingi za binadamu, utu na heshima yake; umuhimu wa kupata huduma bora, mtaji, elimu, afya na teknolojia, ili kujiendeleza na hatimaye, kufikia utimilifu wa maisha ya kibinadamu.

Kuna haja ya kuwana sera na ufahamu makini juu ya umiliki wa mali kwa ajili ya mafao ya wengi na wala si kwa mtu kutaka kujiridhisha binafsi. Watu waliobahatika kuwa na utajiri, wajenge mshikamano wa upendo, utakaowezesha kushirikishana na wengine utajiri huu, kwa kutambua kwamba, mali si kitu, bali hazina kubwa ni ile inayojikita katika uhusiano mwema na jirani.

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kugundua tena udugu katika masuala ya kiuchumi na kuachana na utamaduni wa kumezwa mno na malimwengu pamoja na matangazo ya biashara yanayofanywa na vyombo vya habari.

Athari za myumbo wa uchumi kimataifa, iwe ni fursa ya kutafakari mitindo ya uchumi na maendeleo ili kubadili mifumo ambayo inamtumbukiza mwanadamu katika majanga ya maisha. Iwe ni fursa ya kugundua fadhila ya busara, haki, nguvu na kiasi zinazowaunganisha na wengine kwa kuamiani kwamba, binadamu anapaswa kushirikiana na wengine ili kujenga na kuimarisha Jamii mintarafu utu wa mwanadamu.

Baba Mtakatifu anasema, udugu unazima vita na madhara yake. Kanisa litaendelea kutekeleza wajibu na utume wake kwa kuendelea kuombea amani; kutoa huduma kwa waathirika wa vita; wanaokabiliana na baa la njaa, wakimbizi, watu wasiokuwa na makazi maalum bila kuwasahau wale wanaoishi katika hofu na wasi wasi kuhusu hatima ya maisha yao.

Kanisa, anasema Baba Mtakatifu linapenda kupaaza sauti, ili viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa waweze kusikiliza kilio na mahangaiko ya watu wengi duniani kutokana na uhasama, nyanyaso na uvunjifu wa haki msingi za binadamu, kwani wote ni ndugu. Ni mwaliko wa kujikita katika majadiliano, msamaha na upatanisho ili kujenga tena haki, uaminifu na matumaini mapya sanjari na kuponya madonda ya vita na utengano yanayokwamisha Jumuiya ya Kimataifa kufikia malengo ya kiuchumi na kijamii.

Baba Mtakatifu anawaalika wakuu wa nchi kuridhia mikataba na sheria zinazopiga rufuku matumizi ya silaha za maangamizi ili kulinda maisha ya binadamu. Ni mwaliko wa kuchuchumilia wongofu wa ndani, ili kutambuana kama ndugu, wanaoweza kusaidiana na kufanya kazi na kusimama kidete kulinda na kutetea misingi ya haki na amani.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, rushwa na ufisadi pamoja na uhalifu wa makundi ni mambo yanayotishia udugu. Kukosa na kukoseana ni sehemu ya ubinadamu na kamwe haiwezi kuwa ni sababu ya kumwangamiza jirani yako kutokana na tofauti zenu. Watu wanahamasishwa kujenga msingi ya hakijamii inayotoa uwiano mzuri kati ya uhuru na haki; uwajibikaji wa mt una mshikamano; kati mafao binafsi na mafao ya wengi. Udugu unavunjilia mbali ubinafsi ambao ni chanzo cha mifumo ya rushwa na ufisadi; uhalifu na uvunjifu wa utawala wa sheria; mambo ambayo yanachangia kwa kiasi kikubwa kudhalilisha utu na heshima ya binadamu pamoja na mazingira.

Biashara haramu ya dawa za kulevya ni matokeo ya baadhi ya watu kupenda mno mali na utajiri wa haraka haraka, kielelezo cha kumong’onyoka kwa tunu msingi za kimaadili na sheria jamii. Kuna uchafuzi mkubwa wa mazingira na unyonyaji wa nguvu kazi pamoja na uwepo wa fedha chafu. Mambo haya anasema Baba Mtakatifu yanachangia kuharibika kwa uchumi na mifumo ya kijamii pamoja na kuyatumbukiza mamillioni ya watu katika janga la umaskini.

Huu ndiyo mwelekeo unaofanywa pia katika utumwa mamboleo, biashara haramu ya binadamu, dhuluma na nyanyaso kwa watoto wadogo; wahamiaji. Yote haya ni mambo yanayohitaji wongofu wa ndani, ili kupata maisha mapya. Hali ya wafunga magerezani inatisha, kielelezo cha kukiukwa kwa haki msingi za binadamu, hali inayopaswa kurekebishwa mapema iwezekanavyo.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa siku ya kuombea amani kwa Mwaka 2014 anaendelea kukazia kwamba, udugu unalinda na kutunza mazingira ambayo ni zawadi ya kazi ya uumbaji kwa binadamu. Watu wajitahidi kujenga utamaduni wa kulinda na kutunza mazingira kwa ajili yao na kwa ajili ya kizazi kijacho.

Wakulima watekeleze wajibu wao msingi kwa kuzalisha chakula cha kutosha ili kulisha umati mkubwa wa watu duniani. Kuna uzalishaji mkubwa wa chakula, lakini bado kuna mamillioni ya watu yanakufa kwa baa la njaa! Hii ni kashfa ya karne ya ishirini na moja! Pengo kati ya matajiri na maskini linaendelea kuongezeka maradufu, kumbe kuna haja kwa watu kujikita katika kudumisha misingi ya haki, usawa na kuheshimiana, daima wakisimama kidete kutafuta na kulinda mafao ya wengi.

Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha ujumbe wake kwa siku ya 47 ya kuombea amani kwa Mwaka 2014 kwa kuwataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema kutoa kipaumbele cha kwanza kwa: Mungu na binadamu; kwa kujenga na kudumisha upendo wa kidugu kama sehemu ya mchakato wa kumwendeleza binadamu na kudumisha amani.

Ujumbe huu umehaririwa na
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

No comments:

Post a Comment