Saturday, October 25, 2014

Dhana ya ndoa na familia mintarafu Mafundisho ya Kanisa Katoliki

Baada ya kufanya tafakari ya kina kuhusu dhana ya Ndoa na Familia katika Maandiko Matakatifu, yaani tangu Agano la Kale hadi Agano Jipya, Ninakualika sasa kuendelea kujiunga nami katika tafakari hii, tukijikita zaidi katika Mafundisho ya Kanisa, kwa kuangalia Mitaguso na Nyaraka mbali mbali za kichungaji ambazo zimetolewa na Mababa wa Kanisa katika mchakato wa kuimarisha ndoa na familia, ili ziweze kutekeleza wajibu wake ndani ya Kanisa na Jamii kwa ujumla. RealAudioMP3

Karne ya kumi na tano tunakutana na Mtaguso wa Trento.

Kazi ya madaraka fundishi ya Kanisa (Magisterium) ni kufundisha na kuhakikisha wana kanisa na wote wenye mapenzi mema wanaishi kwa kufwata ufunuo wa maandiko matakatifu. Ndio wenye madaraka ya kutoa maelezo sahihi pale ufunuo wa maandiko unapotokea kutoeleweka katika mazingira ya wakati fulani.
Ikumbukwe kuwa Mtaguso wa Florence wa 1439 ulishaitaja ndoa kama Sakramenti ya saba katika mpangilio wa sakramenti za Kanisa inayoonyesha uhusiano wa Kristo na Kanisa (Efeso 5:32). Kwa malengo ya uzazi na malezi ya watoto, kwa malengo ya uaminifu wa wana-ndoa na kwa ajili ya muungano na umoja wa wana-ndoa usiovunyika
Wana mageuzi waliongozwa na Martini Luther, Calvin na wenzake walifundisha kuwa:
    ndoa iliwekwa kwa ajili tu ya kutimiza au kukabiliana na tamaa za mapenzi, kama kinga (satisfaction of concupiscence)

    Pili walifundisha kuwa ndoa sio Sakramenti, walisema hakuna mahali ambapo imeandikwa kila anayechukua mwanamke anajipatia neema kwa Mungu au kwamba Mungu anaonyesha ishara yeyote kwa wenye ndoa.

    Kushuhudia ndoa kama wajibu wa kanisa ni ujanja wa kanisa kujinyakulia madaraka ya utawala.


Mtaguso wa Trento ulifundisha kuwa ndoa iliwekwa na Mwenyezi Mungu mwenyewe katika kazi ya uumbaji (Mwanzo 2:24; Efeso5:31) ikainuliwa kuwa Sakrmenti na Yesu kristo. Hivyo tukisema ni kwa ajili ya kuondoa tamaa za kimapenzi zilizoletwa na dhambi mbona ndoa iliwekwa kabla ya mwanadamu kuanguka dhambini (Mwanzo 3).
Umoja usiogawanyika wa wana-ndoa unaleta neema na kuwatakatifunza wana-ndoa kama zinazofanya Sakramenti nyingine ili wanandoa waweze kutimiza majukumu yao ya ndoa kwa jina Kristo na kanisa lake.
Na mwisho ifahamike kwamba kanisa ndilo lenye madaraka ya kuadhimisha sakramenti kwani ni mwili wa kristo unaendeleza utume wa Kristo. Hivyo ili ndoa iwe halali isiwe na vizuizi, iwe na kibali cha hiyari lakini iwe na mashahidi rasmi wa kanisa.
Tunapotambua umuhimu wa sakramenti kwanini bado wengi hawapendi kushuhudua ndoa zao makanisa? Je, bila neema ya sakamenti tutafika? Tuungane na kwaya moja iliyoimba “neema ya Sakramenti imefunika madhaifu yenu” kweli ndoa zifunike madhaifu yetu zitusaidie katika utakatifu, kama Mtaguso wa pili wa Vatican unavyotualika katika utakatifu sisi wote.

Kutoka Studio za Radio Vatican ni Mimi Pd. Raphael Mwanga kutoka Jimbo Katoliki la Same, Mwanafunzi wa Ndoa na Familia katika Taasisi ya Ndoa na Familia, Chuo Kikuu cha Kipapa cha Laterano, Roma.
 

No comments:

Post a Comment