Tuesday, October 14, 2014

Fungueni mioyo yenu wazi ili mweze kuona ishara za nyakati za Mungu -Papa


Msibaki mmejifungia katika sheria na kanuni zenu.lakini ifunueni mioyo wazi kwa maajabu ya Mungu, ili mpate kuziona ishara za nyakati. Ni msisitizo uliotolewa na Papa Francisko, wakati wa Ibada ya Misa, Jumatatu hii, mapema asubuhi, katika Kanisa dogo la Mtakatifu Marta ndani ya Vatican. Papa alieleza wakati akitoa ufafanuzi juu ya maneno ya Yesu kwa wanasheria, kama ilivyosomwa katika Injili ya Mtakatifu Luka. Papa alitoa wito kwa waamini kutobaki wamegandamana na sheria na mawazo yao wenyewe, lakini watembee na Bwana siku zote, katika kutafuta mambo mapya.

Papa alizungumzia kifungu hiki cha Injili ambamo Yesu akizungumza na wanasheria, walimtaka atoa ishara ya kudhihirisha ukweli wa yale aliyokuwa akiyasema. Yesu aliwakemea na kuwaita kizazi cha watu waovu.
Papa Francisko, alifafanua juu ya maajabu ya kushtukiza ya utendaji wa Mungu, akisema, mara nyingi, walimu hao wa sheria walimtaka Yesu atoe ishara nae Yesu aliwakemea kwa kushindwa kuziona ishara za nyakati. Papa alisema walimu hao wa sheria hawakuzielewa ishara za nyakati, na waliendelea kudai ishara nyingine za maajabu. Na Yesu aliwahoji kwa nini wanashindwa kuziona ishara hizo au kuzielewa? Papa amesema, awali ya yote, kwa sababu wao walikuwa wameifungia akili yao katika mfumo wao , ambamo walizisoma sheria vizuri na kuzifuata. Wayahudi wote alijua nini cha kufanya, na nini hakutakiwa kufanya, na ni upi mwelekeo wa njia yao. Kila jambo lilikuwa limeandaliwa vyema kwa mpangilio. Na ndivyo wao walivyo jisikia kuwa salama.

Lakini kumbe walikuwa wamesahau kwamba, Mungu si Mungu wa sheria, ni Mungu wa maajabu. Kwa upande mwingine, alisema Francisco , hata kwa watu wake, Mungu huwa na maajabu mengi ya kushtukiza, kama alivyo waokoa wana wa Israel kutoka utumwani Misri.
Walimu na wanasheria walisahau Mungu ni Mungu wa maajabu , kwamba Mungu daima ni mpya , na kamwe hajikanushi mwenyewe , na kamwe hana makosa, lakini daima huendelea kuwa Mungu wa maajabu katika maisha yetu. Walishindwa kuelewa kwa kuwa walijifungia katika mambo yao wenyewe, na hivyo ishara nyingi zilizokuwa zikifanywa na Yesu wao hawakuziona, badala yake wakaendelea kumdai ishara nyingine. Walisahau kwamba, maisha ya binadamu ni safari .Ni kutembea katika njia ya Maisha. Na wakati wa kutembea katika njia ya maisha , daima ni kupata mambo mapya, mambo mapya tusiyo yajua bado.

Aliongeza, ni kutembea katika njia, na si ya kujifungia ndaniya sheria zetu mwenyewe, bali kuifuata njia inayoelekeza katika kudhihirisha nyakati za mwisho za ujio wa Bwana. Maisha ni safari kwenye utimilifu wa Yesu Kristo, wakati atakapo kuja mara ya pili. Kizazi hiki kinataka ishara, lakini Bwana anasema, hapatakuwa na Ishara zaidi ya ile ya Yona, ambayo ni ishara ya ufufuo, na utukufu, ambamo pia tunapaswa kutembea ndani yake. 

Habari kwa hisani ya radio vatican

No comments:

Post a Comment