Thursday, October 23, 2014

Pinda achonga na wawekezaji mjini London

Waziri mkuu wa Tanzania Mizengo Pinda amefanya mikutano na wawekezaji kadhaa ambao wanahudhuria mkutano wa uwekezaji barani Afrika ulioanza Jumatatu tarehe 20 Oktoba 2014 kwenye jijini London, Uingereza. Katika mikutano hiyo, Waziri Mkuu alikutana na Mwenyekiti wa Taasisi ya Africa Matters Limited, Baroness Linda Chalker na kujadiliana naye masuala yanayohusu utawala bora.
Pia alikutana wawakilishi wa kampuni ya Price Waterhouse Coopers (PwC) wakiongozwa na Bw. David Tarimo kutoka Tanzania, Bw. John Gibbs (Kanda ya Afrika) na Bi. Anne Eriksson (Kanda ya Afrika Mashariki) na kuzungumza nao masuala ya nishati na gesi asilia, miundombinu na upatikanaji wa rasilmali fedha (mobilisation of resources).
Katika hatua nyingine Waziri Mkuu alikutana na mwanzilishi na mweneyekiti wa kampuni ya Invest Africa, Bw. Robert Hersov pamoja na wenzake wanne na kumweleza Waziri Mkuu nia yao kuwekeza Tanzania kwenye maeneo ya usindikaji mazao, ujenzi wa maghala ya kuhifadhia mazao na ufadhili wa miradi inayokubalika kiuchumi na ambayo ni rahisi kupatiwa mikopo (Bankable projects).
Naye Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Globeleq, Bw. Mikael Karlsson ambapo alimweleza Waziri Mkuu haja ya kampuni hiyo kuzalisha umeme wa upepo kama njia mbadala ya kuongeza nishati hiyo badala ya kutegemea gesi.
Akijibu hoja zao kwa nyakati tofauti, Waziri Mkuu aliwaeleza wajumbe wa timu hizo kwamba Tanzania ni mahali pazuri kwa uwekezaji lakini pia ni lazima pande zote mbili ziwe makini ili kuhakikisha katika kila mradi inapatikana mizania sawia ya maendeleo (win-win situation).
Akizungumza na Bw. Karlsson wa kampuni ya Globeleq Jumatatu, Oktoba 20, 2014, Waziri Mkuu alisema fursa ya kuzalisha umeme wa upepo iko katika mikoa ya Singida, eneo la Makambako (Njombe), Katavi na Rukwa.
“Sasa hivi mbali ya upepo, mnaweza pia kuangalia uzalishaji wa nishati inayotokana na jotoardhi (geo-thermal) katika eneo lililopo kwenye Bonde la Ufa. Kati ya megawati 40,000 zinazotarajia kuzalishwa ndani ya eneo hili, megawati 5,000 ziko kwenye Bonde la Ufa la Tanzania”, alifafanua. Kampuni ya Globelec pia inamiliki pia mitambo ya SONGAS ambayo inazalisha umeme kwa kutumia gesi asilia.
Waziri Mkuu aliwasili jijini London kuhudhuria mkutano wa wakuu wa nchi unaohusu uwekezaji barani Afrika (The Global African Investment Summit – TGAIS) kwa niaba ya Rais Jakaya Kikwete na ameshiriki mjadala huo pamoja na Rais John D. Mahama wa Ghana, Rais Yoweri Museveni wa Uganda, Rais Paul Kagame wa Rwanda.
Waziri Mkuu amefuatana na Naibu Waziri wa Fedha, Bw. Mwigulu Nchemba; Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. Mahadhi Maalim; Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Bw. Charles Kitwanga; Naibu Waziri wa Uchukuzi, Dk. Charles Tizeba na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Bw. Said Mwambungu.

Habari kwa hisani ya radio vatican

No comments:

Post a Comment