Friday, October 31, 2014

Rais Sata kuzikwa tarehe 11 Novemba 2014

Bwana Roland Msiska Katibu mkuu wa Baraza la Mawaziri Zambia anasema, mwili wa Marehemu Rais Sata unatarajiwa kuwasili nchini Zambia, Jumamosi jioni tarehe Mosi, Novemba 2014 na kuzikwa tarehe 11 Novemba 2014, katika Uwanja wa Mabalozi mjini Lusaka. Rais Guy Scott ataongoza protokali, wakati mwili wa Marehemu Sata utakapowasili kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Keneth Kaunda na baadaye mwili wake utawekwa kwenye Kituo cha Mikutano kimataifa cha Mulungushi.

Wananchi wataanza kutoa heshima zao za mwisho kwa Rais Sata kuanzia Jumapili tarehe 2 Novemba 2014. Ibada kwa ajili ya kumwombea Marehemu Rais Sata itafanyika kwenye Uwanja wa Mashujaa, Lusaka hapo tarehe 11 Novemba 2014.

Marehemu Rais Michael Chilufya Sata aliyefariki hivi karibuni Jijini London aliwahi kusema kwamba, atakatofariki dunia, watu wakumbuke kwamba, kuna “Mwanaume aliyekuja kuleta mabadiliko nchini Zambia” kwa kusema “…ndefwaya nga nafwa mukalelanda ati twalikwete abume pantu ndeisa mukuchinja Zambia”. Marehemu Sata alionesha moyo wa uzalendo na majitoleo katika huduma kwa wananchi wa Zambia katika nafasi mbali mbali alizobahatika kudhaminishwa na wananchi wa Zambia, kiasi kwamba, upendo kwa wananchi wa Zambia, ukawa ni wimbo wake wa Taifa.

Alisimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya wale waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa Jamii, akajitambulisha na watu wa matabaka mbali mbali, kiasi kwamba, wengi wakamkubali kuwa kweli ni mtu wa watu!Unyenyekevu ilikuwa ni silaha yake madhubuti na msamaha kwa watu, kwake kilikuwa ni kielelezo cha unyonge; lakini mambo haya mawili yakawagusa watu wengi ndani na nje ya Zambia. Alipenda kuwaona Wazambia wengi wakijikita katika mchakato wa toba, msamaha na upatanisho wa kweli; kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi.

Hivi ndivyo Bwana George Chella, Msaidizi wa Marehemu Rais Sata katika habari na mahusiano ya kijamii anavyomkumbuka Marehemu Rais Sata enzi ya uhai wake. Kwa mila na tamaduni nyingi za Kiafrika wakati wa maombolezo, watu wanapenda kusimulia mazuri ya yule ambaye ametangulia mbele ya haki, kwa kutambua kwamba, kama binadamu alikuwa na mapungufu yake, lakini si kazi yao kumhukumu, bali Mwenyezi Mungu ndiye hakimu mwenye haki kwani binadamu anababaisha tu!

Wananchi wa Zambia wanaomboleza kwa kuondokewa na Rais wao, waliyemtegemea kuwavusha katika bonde la umaskini, ujinga na maradhi, ili hatimaye, Zambia iweze kucharuka kwa maendeleo endelevu. Mambo aliyoyasimamia katika kipindi cha miaka mitatu ya Urais wake!

Habari kwa hisani ya radio vatican

No comments:

Post a Comment