Thursday, October 23, 2014

Tanzania inaendelea kujinadi kwa walimwengu baada ya kusherehekea miaka 50 ya Uhuru na Kazi!


Waziri mkuu wa Tanzania Mizengo Pinda amezindua jarida la kimataifa la FIRST ambalo limesheheni taarifa za kuitangaza Tanzania kwa wadau wa nchi mbalimbali duniani huku likielezea hatua mbalimbali za ustawi kwa miaka 50 tangu Tanzania ipate ijipatie uhuru wake kutoka kwa Mwingereza.
Uzindusi huo ulifanyika kwenye ofisi za ubalozi wa Tanzania jijini London, Uingereza ambako pia Waziri Mkuu alikabidhiwa nakala ya kwanza ya toleo la sasa ambayo iliwekwa kwenye jalada jekundu la ngozi. Akizungumza katika uzinduzi huo, Waziri Mkuu alisema Serikali ya Tanzania imepata fursa nzuri ya kujinadi kwa watu maarufu na wafanyabiashara wa kimataifa duniani kupitia jarida hilo na akataka uwekwe utaratibu wa kujinadi kisekta.
Alimtaka Balozi wa Uingereza, Bw. Peter Kallaghe aweke mkazo na kusimamia suala hilo ili kuhakikisha matoleo yanayofuata yanakuwa ya kisekta zaidi. “Balozi hapa umefanya kazi nzuri sana ya kuinadi nchi yetu, wala usichoke. Tujitahidi sasa kila mwaka waandike kuhusu fursa za uwekezaji kwa miradi ya kisekta kama utalii, nishati, madini na kadhalika,” alisema.
Waziri Mkuu alimshukuru Mwenyekiti wa taasisi ya First, Bw. Rupert Goodman kwa kazi nzuri aliyoifanya kwa ajili ya Taifa la Tanzania. “Kazi uliyoifanya ni nzuri lakini katika tolea lijalo tuangalie jinsi ya kuitangaza miradi ya uwekezaji ambayo inauzika na iende sekta kwa sekta. Ukisirikiana na Balozi wetu hapa, lazima utapata kitu kizuri,”alisema.
Mapema, akielezea kuhusu jarida hilo la FIRST, Balozi Kallaghe alisema jarida hilo linasambazwa kwenye mashirika mbalimbali ya ndege kama vile British Airways, Air Astana, Lufthansa, United Airlines, Gulf Air, American Airlines, South African Airways, Korean Airways, Etihad Airways, Qatar Airways na Continental Airlines.
“Siyo tu kwamba linasambazwa katika mashirika haya ya ndege, bali pia linawekwa kwenye vyumba vya kupumzikia (First Class and Business Class Lounges) abiria wa daraja la kwanza na la pili wa mashirika haya kwenye viwanja vingi vya ndege,”alisema.
Alisema hili ni toleo la sita ambalo limeandaliwa kwa ushirikiano na ofisi yake (Ubalozi wa Uingereza) ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania lakini pia ikilenga kutangaza fursa za uwekezaji lakini pia ikitangaza hatua mbalimbali za maendeleo ambazo nchi hii imepitia.
Uzinduzi huo ulihudhuriwa pia na Naibu Waziri wa Fedha, Bw. Mwigulu Nchemba; Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. Mahadhi Maalim na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Bw. Charles Kitwanga. Wengine ni Naibu Waziri wa Uchukuzi, Dk. Charles Tizeba na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Bw. Said Mwambungu ambao pia wamefuatana na Waziri Mkuu.

Habari kwa hisani ya radio vatican

No comments:

Post a Comment