Thursday, October 23, 2014

Watu wanateseka kutokana na athari za ugonjwa wa Ebola!



Askofu Anthony Falla Borwah wa Jimbo Katoliki la Gbarnga, Liberia, amewataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuonesha mshikamano wa dhati na wananchi wa Liberia ambao wamekumbwa na ugonjwa wa Ebola, ili wawezde kupata matumaini na kusonga mbele licha ya mateso na changamoto wanazokabiliana nazo kutokana na madhara ya ugonjwa wa Ebola. Anasema kuna watu wanaoendelea kupoteza maisha yao kutokana na magonjwa na njaa lakini kuna kundi kubwa la watu ambao wamekata tamaa ya maisha.

Askofu Borwah anaiomba Jumuiya ya Kimataifa kujifunga kibwebwe ili kuwasaidia watu walioathirika kutokana na maambukizi ya ugonjwa wa Ebola huko Afrika Magharibi. Watu wanakabiliwa na baa la njaa na kwamba, shughuli za kiuchumi na kijamii zinaendelea kudorora kutokana na hofu ya maambukizi ya ugonjwa wa Ebola, ambao kwa sasa umekuwa ni tishio kubwa kwa Jumuiya ya Kimataifa. Kutokana na hofu ya ugonjwa wa Ebola, utu na heshima ya binadamu vinaanza kuwekwa rehani; watu wanashindwa kufarijiana kutokana na majonzi makubwa yanayowasibu kwa wakati huu.

Askofu Borwah anaiomba Jumuiya ya Kimataifa kuendelea kufanya utafiti wa kina ili kubainisha chanzo cha ugonjwa wa Ebola na jinsi ambavyo watu wanaweza kupatia kinga na hatimaye tiba, ili watu waweze kutambua na kuonja tena umuhimu wa zawadi ya maisha. Kanisa linaendelea kuchangia kwa hali na mali katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ebola, kwa kujiwekea mikakati ya muda mrefu na mfupi kwa siku za usoni. 

Habari kwa hisani ya radio vatican

No comments:

Post a Comment