Saturday, November 8, 2014

Tembeeni ili kujenga familia, kutunza mazingira na kutafuta mafao ya wengi!

Chama cha Skauti nchini Italia kina mchango mkubwa katika maisha na utume wa Kanisa kwani kinawashirikisha vijana kushuhudia na kumwilisha Injili katika mazingira yao, kwa kutambua kwamba, kwa kufanya hivi wanashiriki ile dhamana inayobubujika kutoka katika Sakramenti ya Ubatizo; ili kujenga na kudumisha upendo wa kidugu kwa Mungu na jirani pamoja na kutoa huduma makini kwa Kanisa na Jamii katika ujumla wake.

Skauti wanahamasishwa na Mama Kanisa kufanya hija ili kujenga familia, kuheshimu mazingira pamoja na kuimarisha mshikamano wa dhati, kwa kutambua kwamba, Familia ni kiini cha majiundo ya binadamu; jumuiya ya upendo na maisha; mahali ambapo kila mtu anajifunza kushirikiana na wengine na katika dunia. Ni kwa njia ya familia kwamba, Skauti hao wanaweza kuhusiana na wengine katika maisha yao na kwamba, miito mbali mbali inapata chimbuko lake katika familia na hatimaye kuacha chapa ya kudumu katika maisha ya mtu. Dhamana ya familia katika kutoa elimu ni jambo la msingi kabisa.

Haya yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko wakati alipokuwa anazungumza na Chama cha Vijana wa Skauti kutoka Italia, Jumamosi tarehe 8 Novemba 2014. Kwa vijana wa Skauti wao wanapaata dhamana ya majiundo kutokana na Sakramenti ya Ndoa, ili kuwafunda watoto wao katika medani mbali mbali za maisha; huku wakisaidiana katika imani na kutafuta mafao na ustawi wao kama familia. Watoto wakithaminiwa wanaweza kuchangia kuhamasisha upendo na mshikamano ndani ya familia, mwaliko wa kujikita katika majadiliano ndani ya familia pamoja na kupembua changamoto za maisha katika ukweli na uwazi; amani na utulivu, ili familia iweze kupata utulivu na hatimaye, kusonga mbele.

Baba Mtakatifu anawataka Skauti na watu wote wenye mapenzi mema kushiriki katika mchakato wa kulinda na kutunza mazingira, kwani hii ni sehemu ya urithi wa kiimani unaopata chimbuko lake katika Maandiko Matakatifu, kwani kila kiumbe kinaonesha chapa ya Mwenyezi Mungu, aliyemuumba mwanadamu kwa sura na mfano wake. Skauti wanachangamotishwa kuwa na matumizi bora ya rasilimali kwa kuepukana na ulaji wa kupindukia pamoja na kushirikiana na maskini pamoja na wahitaji mbali mbali.

Baba Mtakatifu anawataka Skauti kuwa ni chachu inayojikita katika kutafuta mafao ya wengi, kwa kujishikamanisha na tunu msingi za maisha ya Kiinjili ili kukabiliana kikamilifu na changamoto zinazoibuliwa kutoka kwenye tamaduni mbali mbali; ili kuwa ni vyombo vya Uinjilishaji; huku wakionesha uaminifu wao kwa Kristo na binadamu pamoja na kuendelea kusikia uwepo wa Mungu kati yao.

Mwishoni, Baba Mtakatifu anawataka Skauti kuendelea kutembea huku wakiwa na matumaini kwa kesho iliyo bora zaidi kwa kuthamini majiundo wanayopata shuleni; kwa kukazia nidhamu, ili waweze kuwa kweli ni Wamissionari hodari wa Kristo, kwa kusikiliza kwa makini Neno lake, maisha ya Sala pamoja na kutambua kwamba, wao ni mawe hai ya ujenzi wa Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa.

Habari kwa hisani ya radio vatican

No comments:

Post a Comment