Saturday, November 8, 2014

Kuanguka kwa Ukuta wa Berlin, miaka 25 iliyopita!


Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Miaka 25 tangu Ukuta wa Berlin ulipoanguka kwa kishindo kikubwa bila hata watu kumwaga damu! Mabadiliko haya makubwa katika historia ya Bara la Ulaya ni sehemu ya mchango uliotolewa kwa namna ya pekee na Rais wa Urussi wakati huo Mikhail Gorbaciov na kwa upande mwingine, Papa Yohane Paulo II, aliyewataka watu kutoogopa!

Ukuta wa Berlin ni kielelezo cha ukomunisti uliowagawa wananchi wa Bara la Ulaya, kiasi hata cha kuchukiana na kudhaniana vibaya. Hiki kikawa ni kikwazo cha mchakato wa maendeleo endelevu, kiroho na kimwili, mkwamo wa mchakato wa maendeleo ya kiuchumi na kisiasa. Ukuta wa Berlin ni kielelezo pia cha vita baridi iliyojitokeza mara tu baada ya Vita kuu ya Pili ya Dunia, ulimwengu ukagawanyika katika makundi mawilina hapo pia ukawa ni mwanzo wa kuibuka kwa Umoja wa Nchi zisizofungamana na upande wowote.

Ukuta wa Berlin ulikandamiza tunu msingi za maisha ya binadamu; ukawa ni kikwazo kikuu cha demokrasia na mzunguko wa watu na mawazo; haki msingi za binadamu, utu na heshima ya binadamu vikawekwa rehani na hapo mashindano ya silaha, ili kupimana nguvu yakazuka kwa kasi ya ajabu. Katika kipindi hiki kigumu katika historia ya maisha ya wananchi wa Bara la Ulaya, Vatican na Ufaransa zilizchangia kwa kiasi kikubwa katika majadiliano ya kidiplomasia, kwa kuhamasisha umuhimu wa kusimama kidete kutetea na kudumisha uhuru, haki msingi za binadamu na umoja na mshikamano kati ya watu.

Kunako mwaka 1978, Karol Wojtyla, akachaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki, kiongozi aliyeonja adha ya Pazia la Chuma, huu ukawa ni mwanzo wa cheche za mapinduzi Ulaya ya Mashariki, kwa kukazia mshikamano kati ya watu. Papa Yohane Paulo II akakazia kwa namna ya pekee majadiliano na ushirikiano kati ya Serikali na Kanisa wakati alipofanya hija yake ya kwanza ya kichungaji nchini Poland kunako mwaka 1979. Alitambua mapungufu yaliyokuwa yamejitokeza katika mfumo wa Kikomunisti, kwa kuwa na mwono tenge kuhusu mwanadamu pamoja na kujenga jamii inayoelea kwenye ombwe!

Dr. Joaquin Navarro-Valls, Msemaji mkuu wa Vatican kwa wakati huo, anafafanua kwamba, Rais Mikhail Gorbaciov alikiri mwenyewe kwamba, bila uwepo na mchango wa Papa Yohane Paulo II, kuanguka kwa Ukuta wa Berlin ingelikuwa ni ndoto ya mchana! Rais Gorbacion alisoma kwa makini mchango wa Baba Mtakatifu Yohane Paulo II katika Mafundisho Jamii ya Kanisa, akajichotea utajiri mkubwa, uliomsaidia kuwa na mwelekeo mpya katika kuharakisha mapinduzi ya kisiasa nchini mwake. Papa Yohane Paulo II alikazia pamoja na mambo mengine, uhuru na ukweli; demokrasia, utu na heshima ya binadamu.

Ilikuwa ni tarehe 9 Novemba 1989 umati wa watu kutoka Ujerumani ya Mashariki ulipovuka ukuta, huku bunduki zikiwa zimeinamishwa chini, Urussi ikashindwa kuingilia masuala ya ndani ya Ujerumani na Askari wakapewa amri ya kubaki majumbani mwao. Viongozi wakuu wa nchi mbali mbali wakapigwa butwaa, huo ukawa ni mwanzo wa ukurasa mpya wa historia ya Bara la Ulaya. Ujerumani ikaungana tena na nchi nyingi zilizokuwa chini ya utawala wa Kisovieti zikaanza kuporomoka kama matofali ya kuchoma".

Tarehe Mosi, Desemba 1989 Rais Mikhael Gorbaciov akakutana na Mtakatifu Yohane Paulo II mjini Vatican; mipaka ya Ujerumani ikachorwa upya, vita baridi, vikahifadhiwa kwenye kumbu kumbu za kihistoria na Ukomonisti, ukapelekwa kwenye chumba cha wagonjwa mahututi ie. ICU!

Imehaririwa na
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

No comments:

Post a Comment