Tuesday, October 14, 2014

Hati elekezi kutoka kwa Mababa wa Sinodi kuhusu Familia

Mababa wa Sinodi baada ya kusali, kutafakari na kushirikishana: matatizo, changamoto na fursa mbali mbali katika maisha ya kifamilia kwa muda wa juma zima, Kardinali Peter Erdo, mwezeshaji mkuu, alitoa kwa muhtasari mambo msingi yaliyojadiliwa na Mababa wa Sinodi, hati elekezi katika majumuisho ya maadhimisho ya Sinodi maalum ya Maaskofu kuhusu familia iliyoanza kikao chake hapo tarehe 5 hadi tarehe 19 Oktoba 2014.

Hati elekezi inajikita katika mambo makuu matatu: kusikiliza kwa makini mintarafu hali za kijamii na kitamaduni, katika mazingira ambamo familia zinaishi; kufanya upembuzi yakinifu kuhusu mikakati ya shughuli za kichungaji inayopaswa kuchukuliwa pamoja na kumwangalia Kristo na Injili ya Familia.

Sehemu ya Kwanza ya Hati Elekezi inabainisha kwamba, kimsingi familia ni ukweli na tunu msingi; ni chemchemi ya furaha na kinzani; ni bandari ya mahusiano thabiti lakini wakati mwingine, mahusiano haya yanaacha madonda makubwa katika maisha ya watu. Familia ni shule ya ubinadamu, inayopaswa kusikilizwa kwa umakini mkubwa kwa kuzingatia makando kando yake yanayojikita wakati mwingine katika ubinafsi uliokithiri na upweke wa kutupwa!

Katika mazingira kama haya, Mama Kanisa anatumwa kutoa neno la faraja, kwa kutambua kwamba, binadamu asili yake ni Mungu mwenyewe, changamoto na mwaliko wa kuthamini na kuenzi tunu msingi za maisha ya ndoa na familia. Waamini wahamasishwe kujisikia kuwa ni kiungo muhimu cha maisha na utume wa Kanisa hata kwa wale ambao wakati mwingine wamejikuta wakielemewa na mapungufu yao ya kibinadamu. Hapa waamini wanahimizwa kujitaabisha kuyafahamu kwa kina mafundisho ya Kanisa sanjari na kukimbilia huruma ya Mungu.

Sehemu ya Pili ya Hati Elekezi kutoka kwa Mababa wa Sinodi inamwangalia Kristo na Injili ya Familia mintarafu historia ya ukombozi wa mwanadamu, kwa kuonesha uhusiano wa dhati kati ya mwanaume na mwanamke wanaoshiriki kikamilifu katika mpango wa kazi ya uumbaji inayokamilika kwa kazi ya ukombozi iliyotekelezwa na Kristo mwenyewe. Ikumbukwe kwamba, familia ni sehemu ya mpango wa Mungu tangu kuumbwa kwa ulimwengu.

Mababa wa Sinodi wanawataka waamini kufanya upembuzi yakinifu kwa kuangalia tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, madonda wanayokabiliana nayo pamoja na hali ambazo zinakinzana kimsingi na mafundisho pamoja na Mapokeo ya Mama Kanisa, ili kujenga na kudumisha umoja na mshikamano ndani ya Kanisa. Hapa kinachozungumziwa na uchumba sugu, ndoa za serikali, wanandoa waliotalakiana na kuoa au kuolewa tena. Mama Kanisa anawatambua watoto wake wanaoshiriki katika maisha na utume wake hata kama si katika utimilifu wake. Anatambua na kuheshimu tunu msingi wanazohifadhi katika maisha yao, licha ya mapungufu yao ya kibinadamu.

Mababa wa Sinodi wanakazia ukweli, uzuri wa maisha ya familia na huruma ya Mungu; mambo ambayo yametolewa ushuhuda na Mababa wa Sinodi wakati wa maadhimisho; wanandoa wamekumbana na mawimbi mazito katika maisha ya ndoa na familia, lakini bado wameendelea kushikamana na kupendana kwa dhati. Ni wajibu na dhamana ya Mama Kanisa kuwasindikiza watoto wake ambao ni dhaifu, kwa kuwajengea tena imani na matumaini ili waweze kukabiliana na changamoto za maisha ya ndoa na familia.

Sehemu ya Tatu ya Hati Elekezi inagusia changamoto na mikakati ya shughuli za kichungaji kama sehemu ya mchakato wa utangazaji wa Injili ya Familia kwa Watu wa Mataifa. Mama Kanisa anatumwa kuwatangazia watu mbali mbali katika mazingira yao tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, kwa kutambua kwamba, Uinjilishaji ni dhamana ya Watu wote wa Mungu na kwamba, watu lazima watangaziwe Injili ya Familia na furaha inayoijaza mioyo ya watu.

Hapa kuna haja ya kujikita katika wongofu wa kimissionari; lugha makini, majadiliano yanayosimikwa katika ukweli na uwazi na kwamba Sakramenti ya Ndoa ni utume wenye: haki, dhamana na wajibu. Wanandoa wapya wanapaswa kuandaliwa barabara ili waweze kufikia ukomavu wa kiimani, watambue uzuri na changamoto katika maisha ya ndoa na familia, wafahamishwe kinzani zinazoweza kujitokeza kutokana na masuala ya kiuchumi na kijamii. Waamini walei, wawasaidie wanandoa katika kutekeleza dhamana na maisha yao ndani ya familia.

Mababa wa Sinodi wanasema kwamba, Familia yote ya Mungu inawajibika kuwafunda wanandoa watarajiwa kwa njia ya ushuhuda makini pamoja na kuwapatia mafundisho ya kina kwa kutambua kwamba, kuna uhusiano mkubwa kati ya Sakramenti ya Ndoa na Sakramenti nyingine za Kanisa kama chemchemi ya neema. Kabla ya kufunga ndoa, wanandoa watarajiwa washiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa na kwamba, wanandoa wapya wasindikizwe katika maisha yao ya ndoa na familia katika miaka ya kwanza kwanza.

Mababa wa Sinodi wanasema, Parokia ni mahali muafaka kwa wanandoa wapya kupata majiundo endelevu, kwa kuwahamasisha kupokea na kulea zawadi ya maisha. Wasaidiwe kutambua tasaufi ya maisha ya ndoa na familia, sala na matendo ya huruma. Wanandoa wapya wahamasishwe kushiriki katika Ibada mbali mbali za Kanisa kwa kutambua kwamba, wao pia ni vyombo vya Uinjilishaji.

Mababa wa Sinodi wameona cheche za mambo mema kwa "wachumba sugu", wasaidiwe ili hatimaye, waweze kufikia maamuzi ya kufunga ndoa Kanisani. Ukosefu wa uhakika wa fursa za ajira, mshahara wa kutosha kukidhi mahitaji ya familia ni kati ya mambo yanayopelekea watu wengi kuendelea kuwa katika "uchumba sugu". Watu hawa wasaidiwe kuona na kutambua tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, utume unaopaswa kutekelezwa kwa unyenyekevu na uvumilivu mkubwa, hapa familia za Kikristo zinapaswa kuonesha ushuhuda kama vyombo makini vya Uinjilishaji.

Mababa wa Sinodi kwa moyo wa upendo na mshikamano, wanawaalika viongozi wa Kanisa kuibua mbinu mkakati mpya wa shughuli za kichungaji kwa ajili ya wanandoa waliotalikiana na kuamua kuoa au kuolewa tena; familia ambazo zinakumbana na madonda makubwa katika maisha na utume wake. Matatizo ya kiuchumi, kijamii na kiimani, ni changamoto kwa Makanisa mahalia kuendeleza majadiliano ya kina, ili kujenga na kuimarisha uaminifu kwa Injili ya Familia. Waamini hawa wahudumiwe kwa huruma na mapendo. Wasikilizwe kwa umakini, wapendwe na kuthaminiwa. Bado kuna changamoto kubwa katika ndoa mseto.

Mababa wa Sinodi wanasema, Kanisa ni nyumba inayopaswa kuwakaribisha wote hata wale wanaoishi katika ndoa za watu wa jinsia moja, bila ya kuhatarisha wala kubeza mafundisho tanzu ya Kanisa Katoliki kuhusu ndoa na familia. Hii ni changamoto kubwa katika malezi na majiundo ya waamini. Kanisa halitakubali kushinikizwa na Mashirika ya Kitaifa na Kimataifa ka kisingizio cha usawa wa kijinsia. Waamini watambue matatizo na changamoto za kimaadili zilizoko mbele yao. Haki msingi za watoto zinapaswa kuzingatiwa na walezi wa jinsia moja.

Mababa wa Sinodi wanawahimiza wanandoa kupenda na kuthamini maisha kama kielelezo cha upendo wao. Wafundishwe njia asilia za uzazi ili waweze kufurahia maisha yao ya ndoa, kwa kuheshimu na kuthamini utu na heshima ya binadamu inayojikita katika Injili ya Uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Wanandoa waendelee kupatia majiundo endelevu.

Mababa wa Sinodi wanasema kwamba, elimu na dhamana ya familia ni kati ya changamoto kubwa katika azma ya Uinjilishaji. Familia zijitahidi kuonesha mfano bora wa kuigwa kwa kujenga mazingira bora ya makuzi, urithishaji wa tunu msingi za maisha ya kiroho na kiutu na kwamba, Kanisa litaendelea kuenzi familia katika utekelezaji wa dhamana na utume wake.

Mwishoni Mababa wa Sinodi wanakiri kwamba, hati hii ni matunda ya mchango wa mawazo uliotolewa katika misingi ya ukweli na uwazi; kwa kusikilizana na kuheshimiana na kwamba, tafakari hii iendelee kufanyiwa kazi kwenye Makanisa mahalia, ili Maadhimisho ya Sinodi ya kawaida ya Maaskofu itakayoanza hapo tarehe 4 hadi tarehe 25 Oktoba 2015 iweze kuzaa matunda yatakayoliwezesha Kanisa kutangaza Injili ya Familia.

Imetayarishwa na
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

No comments:

Post a Comment