Wednesday, October 8, 2014

Mkesha wa sala kuombea Sinodi Maalum ya Maaskofu


Jumamosi majira ya saa moja za jioni, makumi ya maelfu ya watu wajumuika katika uwanja wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro , kwa ajili ya mkesha wa sala, ulio ongozwa na Baba Mtakatifu Francisko, kuombea Sinodi Maalum ya Maaskofu, ambayo imefunguliwa Jumapili hii kwa Ibada ya Misa katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro Vatican. Sinodi hii maalum inachambua changamoto cha Kichungaji katika familia, kwenye muono wa Uinjilishaji .

Katika Mkesha huu wa sala, Baba Mtakatifu Francisko,alitoa wito kwa Waamini wawaombee Mababa wa Sinodi , kwa namna ya pekee, zawadi ya kuisikiliza sauti ya Mungu inavyo waambia na kuwa na moyo wa uwazi katika majadiliano na kukaza macho yao kwa Yesu Kristo.

Kabla ya sala ya Mkesha, kulikuwa na utaratibu wa kusikiliza Neno la Mungu , Maandiko Matakatifu, ushuhuda wa wanandoa, maombi, kuimba na tafakari juu ya maandishi ya Papa Francisco na watangulizi wake.

Baba Mtakatifu alisema, ushirikiano katika maisha ya ndoa, uwazi kwa zawadi ya maisha, kulindana, kuheshimiana, kukutana na kumbukumbu ya vizazi vilivyopita, msaada wa elimu, maambukizi ya imani ya Kikristo kwa watoto wao. . .pamoja na mengine, kwa yote hayo , familia inaendelea kuwa shule iliyosimikwa katika ubinadamu , na mchango muhimu katika haki na umoja katika jamii. (Cf. ibid., N. Evangelii gaudium, 66-68).

Na kwa kadri familia inavyozamisha mzizi wake katika kina kirefu cha umoja wa familia , ndivyo inavyo wezekana maisha hayo kuzama zaidi ndani yake bila kupoteza hisia zake katika mambo mageni. Kwa upeo huo, inatusaidia kufahamu umuhimu wa mkutano huu wa Sinodi Maalum ya Maaskofu, inayofunguliwa kesho.

Zaidi ya yote, Papa alisema, tunaomba Roho Mtakatifu awape Mababa wa Sinodi, zawadi ya kusikiliza, kusikiliza kwa namna ya Kimungu, ili wapate kusikia, pamoja naye, kilio cha watu; kusikiliza kilio cha watu hadi waweze kupumua mapenzi Mungu.

Papa aliomba ili kwamba, Maaskofu waweze kupata zawadi ya kusikiliza kwa makini na uwazi katika majadiliano ya kweli, uwazi wa kidugu, wenye kuwawezesha kulibeba jukumu la Kichungaji, na uwajibikaji kwenye hoja za mabadiliko, yanayojitokeza katika nyakati hizi.

Papa alieleza katika hatua hiyo ya kusikiliza na majadiliano juu ya familia, wakiwa pamoja na Kristo, inakuwa ni tukio la Kikudra ambamo wanaweza kufanya upya utendaji kwa mfano wa Mtakatifu Francisco, kwa Kanisa na jamii.

Pamoja na furaha ya Injili, aliendelea kusema, tutaweza kugundua njia ya mapatano, na huruma ya kanisa katika kuwaona maskini na rafiki wa maskini, kwa nguvu ya kanisa inawezekana, kukua katika uvumilivu na upendo, na kuondokana na hofu na changamoto zake, katika yote, ndani ya kanisa lenyewe na nje yake (Lumen Gentium, 8).

Papa alikamilisha kwa kuomba uvuvio wa Roho Mtakatifu, uvume juu ya kazi za Sinodi na Juu ya Kanisa na juu ya Ubinadamu wote. Uweze kufungua vifundo vyote vinavyozuia watu kukutana mmoja kwa mwingine, kuponya majeraha yanayovuja damu , na kufufua matumaini. Bwana na atupatie mbinu hizi za upendo kama Yesu alivyopenda. Na ili ujumbe wetu uweze kuleta uhai na shauku ya Wamisionari wa kwanza wa Injili.

Washiriki wa sinodi hii, wametoka bara zote tano za dunia kuzungumzia changamoto za Kichungaji kwa familia, katika muono wa Uinjilishaji, ni kama ifuatavyo: Kuna Marais wa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki 114, Wakuu wa Makanisa ya Katoliki ya Mashariki 13, Wakuu wa Idara za Curia ya Roma 25, Wajumbe 9 kutoka Sekretariati ya Baraza la kawaida wa Sekretarieti, Katibu Mkuu wa Jimbo la Papa, na katibu mwandamizi, Wajumbe 3 kutoka 3 wanaowakilisha Wakuu wa Mashirika, na wajumbe 26 walioteuliwa na Papa. Washiriki wengine ni pamoja na 8 Mabruda wanane, Wajumbe 38 wakiwa ni wakaguzi, wakimwemo wanandoa 13 wanandoa, na 16 wataalam. Jumla ya idadi ya washiriki wote wa Sinodi ni 253.Sinodi hii ni hatua ya kwanza kwa ajili ya Sinodi ya kawaida ya mwaka kesho 2015, na hivyo itakamilika bila kutoa tamko la mwisho juu yale yaliyojadiliwa, kwa kuwa maoni yatakayotolewa yatafikishwa katika Sinodi ya Kawaida ya mwaka kesho ambayo itatoa hati yenye tamko juu utendaji wa kanisa katika kupambana na changamoto za Kichungaji katika familia. 

Habari kwa hisani ya radio vatican

No comments:

Post a Comment