Tuesday, November 4, 2014

Familia: Changamoto na matumaini yake!


Askofu mkuu Vincenzo Paglia, Rais wa Baraza la Kipapa la Familia anasema, umefika wakati kwa familia kutoka kifua mbele, ili kushuhudia dhamana na utume wake katika maisha ya hadhara. Kanisa linabeba dhamana na wajibu mkubwa wa kuwaonesha walimwengu uhusiano uliopo kati ya Bwana na Bibi katika kuendeleza uzao wa binadamu. Muungano huu ni msingi thabiti katika ujenzi wa Jamii ya binadamu na mahusiano yake.

Askofu mkuu Paglia ameyasema haya wakati wa uzinduzi wa Kongamano la Kumi na Sita la Wakatoliki na Maisha ya Hadhara, lililoandaliwa na Vyama vya Kitume vya Kikatoliki kwa kushirikiana na Mfuko wa Chuo Kikuu cha San Pablo, utakaofanyika Jimbo kuu la Madrid, kuanzia tarehe 14 hadi tarehe 16 Novemba 2014, huku wakiongozwa na kauli mbiu "Familia: changamoto na matumaini".

Jambo msingi anasema Askofu mkuu Paglia kwamba, familia inadhamana ya kuendeleza zawadi ya maisha inayofumbatwa katika Fumbo la upendo kati ya Bwana na Bibi. Hii ni dhamana inayotekelezwa na Familia imara na thabiti na hata zile ambazo zinamadonda na majeraha makubwa katika maisha na utume wao. Hii ni changamoto kwa familia kuhakikisha kwamba, zinajitokeza katika maisha ya hadhara ili kushuhudia utume na dhamana yake katika Jamii, kwa kushirikisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia kama kielelezo cha imani tendaji.

Familia za Kikristo hazina budi kuonesha mshikamano wa dhati na Kanisa, kwani Kanisa ni mlinzi na mtetezi mkuu wa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia ambazo zinapigwa danadana katika ulimwengu mamboleo. Mahusiano kati ya Familia na Kanisa bado hayajapata nguvu sana, mwaliko kwa wanandoa kuimarisha zaidi mahusiano haya, ili kwa pamoja kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika maisha ya ndoa na familia.

Habari kwa hisani ya radio vatican

No comments:

Post a Comment